Imani potofu ya #1: Maziwa fresh yanaponya vidonda vya tumbo
Ni ushauri wa kwanza kabisa wengi hupewa: “Kunywa maziwa, yatatuliza maumivu.”
Lakini ukweli ni huu: maziwa huleta nafuu ya muda mfupi tu — na baadaye, huweza kuzidisha tatizo.
Kwanza, maziwa huchochea uzalishaji wa asidi tumboni baada ya muda mfupi, hali inayochochea zaidi vidonda.
Pili, maziwa huunda utando wa muda mfupi (protein coating) unaofunika vidonda dhidi ya asidi — lakini punde utando huo unapofutika, asidi hurudi kwa nguvu zaidi, na kusababisha vidonda kuumia tena kwa kiwango kikubwa zaidi.
Matokeo? Maumivu makali zaidi, mzunguko wa mateso unaojirudia, na imani potofu inayokuzuia kupata nafuu ya kweli.
Kwahiyo hupaswi kutumia maziwa fresh peke yake kama tiba ya vidonda vya tumbo.
Usinielewe vibaya. Sijamaanisha usitumie kabisa maziwa fresh. Maana yangu ni kwamba mazima fresh peke yake hayawezi kukusaidia kutibu vidonda vya tumbo. Labda kama unachanganya na dawa nyingine hapo sawa.
Imani potofu ya #2: Kushinda njaa kunasababisha vidonda vya tumbo
Wengi huamini kwamba ukikaa muda mrefu bila kula, moja kwa moja utapata vidonda vya tumbo.
Lakini ukweli ni kwamba si njaa inayosababisha vidonda — bali ni uwepo wa bakteria aitwaye H. pylori pamoja na matumizi mabaya ya baadhi ya dawa za kupoza maumivu ya kichwa, tumbo, hedhi n.k
Njaa inaweza kuongeza usumbufu kwa mtu ambaye tayari ana vidonda, lakini haitoshi kusababisha vidonda vyenyewe. Kwahiyo kula kila baada ya muda si suluhisho — kama chanzo halisi hakijashughulikiwa.
Imani potofu ya #3: Msongo wa mawazo unasababisha vidonda vya tumbo
Ni rahisi kuamini kwamba msongo wa mawazo (stress) nao pia husababisha vidonda — kwa sababu mara nyingi unahisi maumivu kuongezeka pindi unapokuwa na wasiwasi au kwenye dimbwi la mawazo.
Lakini ukweli ni huu: Stress haiwezi kusababisha vidonda moja kwa moja. Inaweza kuchangia hali kuwa mbaya zaidi kwa mtu mwenye vidonda tayari, lakini chanzo halisi mara nyingi ni H. pylori au matumizi ya dawa zinazochoma kuta za tumbo (kama dawa za kupoza maumivu ya kichwa, tumbo, hedhi n.k)
Ni kweli kuweka akili yako katika hali ya utulivu na kutokuwa na stress ni muhimu — lakini hiyo pekee haitoshi kuponya vidonda.
Imani potofu ya #4: Kula vyakula vyenye asidi na viungo vingi kunasababisha vidonda vya tumbo.
Wengi huacha kula vyakula vya viungo au vyenye ladha kali kwa hofu kuwa vitazalisha vidonda. Lakini ukweli ni kwamba chakula peke yake hakisababishi vidonda.
Vyakula hivi vinaweza kusababisha usumbufu au kuchochea maumivu kwa wale ambao tayari wana vidonda, lakini havianzi mchakato wa uharibifu wa ukuta wa tumbo na kusababisha vidonda.
Kwahiyo kupangilia au kuchagua aina ya vyakula hakutoshi kukufanya upone vidonda kwasababu vyakula sio chanzo na wala havipelekei mtu kupata au kupona vidonda.
Hivyo basi, kuamini kuwa kubadilisha tu chakula kutatosha kusaidia kutibu vidonda vya tumbo ni kujichelewesha kupona na kuondokana na maumivu ya kila siku yanayokukabili.
Imani potofu ya #5: Vidonda vya tumbo vinaambukizwa
Hii ni dhana ya kutisha — na ya uongo.
Vidonda vya tumbo havipatikani kwa kuambukizwa moja kwa moja kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Kinachoambukiza ni bakteria wa H. pylori — na hata hivyo, si kila mtu aliye na bakteria huyu hupata vidonda. Mchanganyiko wa bakteria, kinga ya mwili, na hali ya mazingira ya tumbo ndiyo huamua.
Kwa hiyo, vidonda si maradhi ya kuambukiza kama mafua.
Imani potofu ya #6: Huwezi kuwa na vidonda vya tumbo pasipo dalili zozote.
Hii ni hatari kwa sababu watu wengi wanakuwa navyo kwa miezi — au hata miaka — bila kujua.
Dalili huweza kujificha au kuchukuliwa poa kama tumbo kujaa gesi, kuvimbiwa, kichefuchefu, au kuchoka tu.
Na kabla hujajua, vidonda hivyo vinakuwa vimesababisha matatizo makubwa kama: kutokwa damu ndani kwa ndani, au hata tundu kwenye tumbo (perforation).
Kutokuwa na dalili hakumaanishi uko salama. Hapa ndipo watu wengi huteleza.