• Home
  • |
  • Blog
  • |
  • Usichokijua Na Unachopaswa Kujua Kuhusu Matangazo Ya Kulipia Mtandaoni!

August 17, 2022

Usichokijua Na Unachopaswa Kujua Kuhusu Matangazo Ya Kulipia Mtandaoni!

Kila Biashara inahitaji wateja. Kwasababu wateja ndio pumzi ya kuifanya biashara yoyote ile iishi. Bila wateja wakufanya manunuzi lazima biashara ife.

Lakini swali la kujiuliza ni kwamba...

“Wateja wa kufanya manunuzi ya bidhaa au huduma yako unawapataje?”

Ifahamike kwamba upatikanaji wa wateja haujawahi kuwa rahisi hata siku moja.

Ndio maana biashara nyingi zinakufa kila iitwayo leo kwasababu tu ya ukosekanaji wa wateja.

Nisikilize kwa makini...

Kuna njia nyingi ambazo mtu anaweza akazitumia kupata wateja lakini zilizo nyingi sio tegemezi.

Nikisema sio tegemezi namaanisha upatikanaji wa wateja kwa njia hizo ni wa mawazo sana na sio wa uhakika.

Lakini ipo njia moja ambayo ni ya uhakika na tegemezi.

Kwa kutumia njia hii unakuwa na uhakika wa kupata wateja kila siku, kila wiki, kila mwezi na muda wowote katika mwaka mzima.

Njia hiyo ni ipi? Swali zuri.

Njia hiyo ni MATANGAZO YA KULIPIA MTANDAONI.

Matangazo ya kulipia mtandaoni ni njia ya haraka na ya uhakika wa kupata wateja idadi unayoitaka muda wowote.

Pengine unajiuliza...

Nini Maana Ya Matangazo Ya Kulipia Mtandaoni?

 Maana ya matangazo ya kulipia mtandaoni ni kulipa pesa kwenye mtandao husika (mfano: Facebook au Instagram) ili mtandao huo ukukutanishe wewe na watu ambao wana sifa za kuwa wateja wa bidhaa au huduma yako.

Au kwa lugha rahisi unaweza ukasema ni kununua watu ambao wana sifa za kufanya manunuzi ya bidhaa au huduma yako.

Hiyo ndio maana halisi ya kufanya matangazo ya kulipia.

Wengi wanajua kufanya matangazo ya kulipia ni kupata wateja. Ndio lengo la kufanya matangazo ya kulipia ni kupata wateja lakini hiyo sio maana sahihi ya matangazo ya kulipia kwasababu unaweza ukafanya matangazo ya kulipia na bado usipate wateja.

Upatikanaji wa wateja ni MCHAKATO na sio Tukio tu kama kugusa swichi ya umeme.

Kwahiyo kwa maelezo rahisi ni kwamba...

Lengo la matangazo ya kulipia ni kukukutanisha wewe na watu ambao wana sifa za kuwa wateja wako ili uwapitishe kwenye mchakato wa kuwafanya wawe wateja wako.

Tambua kwamba “Kila mtu ni mteja lakini mteja wako wewe sio kila mtu”

Kwahiyo Kwakuwa mtandaoni kuna watu tofauti tofauti, ukifanya matangazo ya kulipia mtandao husika unakusaidia kulifikisha tangazo lako kwa watu wenye sifa ya kuwa wateja wako ili wakutafute uwapitishe kwenye mchakato wa kuwafanya wawe wateja wako.

Matangazo ya kulipia mtandaoni yana faida zipi? Zifuatazo ni...

Faida Za Matangazo Ya Kulipia Mtandaoni!

Faida ya #1: Ukifanya matangazo ya kulipia mtandaoni unao uwezo wa kuamua tangazo lako liwafikie watu wa eneo fulani tu.

Hii inakua ni tofauti kufanya matangazo kwa njia kama TV, Redio au magazeti.

Kwa njia hizi haiwezekani kabisa kuamua kwamba unataka tangazo lako liwafikie watu wa eneo fulani pekee.

Tangazo lako likitangazwa kwenye TV kila mtu ambaye ana TV na chaneli husika haijalishi yupo eneo gani lazima tangazo lako ataliona.

Kwahiyo kwa njia hizi unaweza ukajikuta tangazo lako linatangazwa hata sehemu ambazo wewe binafsi huwezi ukafikisha bidhaa au huduma yako.

Hivyo utajikuta unapoteza hela yako bure.

Tuendelee na...

Faida ya #2: Ukifanya matangazo ya kulipia mtandaoni unao Uwezo wa kuamua umri wa watu ambao unataka walione tangazo lako.

Hii inakua tofauti kwa njia kama TV, Redio au magazeti.

Kwa njia hizi haiwezekani kabisa kusema kwamba tangazo lako litatazamwa na watu wa umri fulani.

Kwa njia hizi tangazo lako litamfikia mtu wa umri wowote ule.

Kwahiyo kwa kutumia njia hizi unaweza ukajikuta tangazo lako linatazamwa na watoto ambao hata sio wateja wako lengwa kitu ambacho kitafanya upoteze hela yako bure bila kupata matokeo mazuri.

Faida ya #3: Ukifanya matangazo ya kulipia mtandaoni unao Uwezo wa kuamua tangazo lako liwafikie watu wa jinsia (gender) fulani.

Unaweza ukaamua tangazo lako liwafikie wanawake tu au wanaume tu au wote kwa pamoja.

Lakini kwa hizi njia zingine haiwezekani kabisa.

Labda nikuulize swali...

Hivi unaweza ukapeleka tangazo lako kwenye kituo Cha Redio halafu ukawambia unataka tangazo lako liwafikie wanawake tu?

Jaribu uone kitakachotokea.

Sio kidogo wataenda kukupima akili au kukuombea kabisa.

Tunaelewana mpaka hapo?

Basi tuendelee na faida ya nne.

Faida ya #4: Ukifanya matangazo ya kulipia mtandaoni unao uwezo wa kuamua tangazo lako liwafikie watu wanaopendelea bidhaa au huduma yako pekee na wakati kwa kutumia njia hizo zingine haiwezekani kabisa.

Tukimalizia faida ya mwisho

Faida ya #5: Ukifanya matangazo ya kulipia mtandaoni unao uwezo wa kuamua tangazo lako liwafikie watu wa idadi fulani unayoitaka wewe.

Hii ni tofauti na kwenye redio, TV au magazeti. Kwa kutumia njia hizo huwezi ukaamua tangazo lako liwafikie watu wa idadi unayoitaka wewe.

Kwahiyo kwa kufanya matangazo ya kulipia mtandaoni ni rahisi Sana na haraka kupata wateja wa bidhaa au huduma yako tofauti na njia hizo zingine.

Unanielewa rafiki yangu? Vizuri.

Sasa, kabla hatujafika mbali kuna kitu cha msingi sana ningependa nikwambie.

Kitu hicho ni kwamba...

Unatakiwa uelewe kufanya matangazo ya kulipia kwenye mitandao ya kijamii hakuna utofauti kabisa na fundi wa kushona nguo.

Ninamaanisha nini? Ninachokimaanisha ni hiki hapa... Unavyoenda kwa fundi wa nguo, lazima umpatie fundi huyo maelekezo ya namna gani unataka akushonee nguo yako.

Fundi hatajua nguo yako inashonwaje endapo hujampatia maelekezo kamili.

Hivyo basi hata kwenye matangazo ya kulipia mtandaoni lazima uuambie mtandao husiki kwamba lengo lako la kutaka kufanya matangazo ni lipi ili uhakikishe unakusaidia wewe kutimiza lengo lako.

Kuna malengo mengi ya kufanya matangazo ya kulipia. Kwa Lugha ya kimtandao malengo hayo yanaitwa...

Madhumuni (Objectives) Ya Kufanya Matangazo Ya Kulipia.

Kumbuka maana halisi ya kufanya matangazo ya kulipia mtandaoni ni kukutanishwa na watu ambao wana sifa za kuwa wateja wako.

Sasa unataka baada ya kukutanishwa na watu ha, watu hao wafanye nini?

Naomba ieleweke kwamba kabla ya watu hawa kukutana na wewe kabisa wanakutana na Tangazo lako mtandaoni. Kwahiyo lazima uuambie mtandao husika unachotaka watu hawa wakifanye baada ya kuliona tangazo lako.

Hicho ambacho utauambia mtandao ukutimizie kwa watu hawa watakaoliona tangazo lako wafanye nini ndicho kinachoitwa dhumuni la kufanya matangazo ya kulipia.

Kwa lugha rahisi ni kwamba...

Dhumuni la tangazo ni kuamua nini unataka msomaji wa tangazo lako afanye baada ya kuliona au kulisoma tangazo lako!

Kwa kuamua kitendo ambacho unataka msomaji wa tangazo lako afanye baada ya kuliona au kulisoma tangazo lako inakua rahisi kwa mtandao husika (Facebook au Instagram) kuweza kulifikisha kwa watu husika ambao wana sifa na tabia ya kufanya kitendo hicho wakiwa mtandaoni!

Mfano wa kitendo hicho yaweza kuwa...

  • kukutumia Meseji
  • kukupigia simu
  • kuangalia video
  • kuja WhatsApp
  • kucomment, like na kushare n.k

Kwahiyo unapochagua dhumuni la tangazo lako mtandao husika unahakikisha unalifikisha tangazo lako kwa watu ambao wana sifa na tabia za kufanya kitendo ambacho wewe unakua umeamua msomaji afanye baada ya kuliona au kulisoma tangazo lako.

Kwa mfano: kama dhumuni lako utaweka mteja kukutumia meseji maana yake ni kwamba...

Mtandao utalifikisha tangazo lako kwa watu ambao wana sifa na tabia ya kutuma meseji kwa wafanyabiashara wa biashara kama yako ili kuhakikisha unapata matokeo makubwa na watu sahihi.

Tuko pamoja mpaka hapo rafiki?

Tunaendelea...

Kwa hapa Tanzania mitandao mikubwa ambayo itakuletea matokeo makubwa ukifanya matangazo ya kulipia ni Facebook na Instagram.

Uzuri ni kwamba mitandao hii 2 yote inamilikiwa na mtu mmoja kwahiyo unaweza ukafanya tangazo lako lionekane kwa watu wa Facebook na watu wa Instagram kwa wakati mmoja kwa Kutumia dhana (tool) ya kufanya matangazo inayoitwa Ads manager!

Kama unatumia Laptop kuipata Dhana hii search...

business.facebook.com

Na endapo unatumia simu kuipata Dhana hii nenda play store au app store Kisha download na uinstall app hii inaitwa *Meta Ads manager*

Sasa...

Wakati unataka kufanya *sponsored ads* (tangazo la kulipia) kwa Kutumia ads manager utagundua kuna makundi 3 ya madhumuni ya tangazo.

Madhumuni hayo ni...

  • Awareness
  • Consideration
  • Conversion
Mr Bokko's Facebook Ad Obj Image

Kama unavyoweza kuona kwenye picha ya hapo juu kuna makundi 3 ya madhumuni ya tangazo.

Lakini Kila dhumuni Lina vipengele vyake.

Hii inamaanisha Nini?

Inamaanisha kwamba hivyo vipengele kwa Kila dhumuni moja ni kitendo husika ambacho msomaji wa tangazo lako atafanya baada ya kuliona au kulisoma tangazo lako.

Kwenye dhumuni la Awareness una...

    1. Brand awareness

    2. Reach

Kwenye dhumuni la consideration una...

    3. Traffic

    4. Engagement

    5. App installs

    6. Video views

    7. Lead generation

    8. Messages

Kwenye dhumuni la conversion una...

    9. Conversions

   10. Catalog sales

   11. Store traffic

Hayo ndio madhumuni 11 ya kufanya matangazo ya kulipia (sponsored ads)

Ngoja tuanze na dhumuni moja baada la lingine.

AWARENESS

Hapa kwenye awareness dhumuni ni kuongeza ufahamu wa biashara yako kwa watu.

Yaani kama unataka biashara yako ifahamike kwa watu wengi dhumuni lako linakua hili la awareness.

Kwenye dhumuni hili unaweza ukachagua....

     1. Brand awareness!

Kama ukichagua kipengele hiki maana yake mtandao utalifikisha tangazo lako kwa watu ambao wana sifa na tabia za kupenda kufahamu zaidi kuhusu biashara fulani.

Hapa tangazo lako linakua ni logo ya biashara yako ili Kujitangaza kwa watu wakufahamu zaidi.

Kwahiyo lengo ni kuongeza au kukuza ufahamu wa biashara yako na sio kupata wateja.

Lakini pia unaweza kuchagua kipengele Cha...

    2. Reach.

Kama ukichagua kipengele hiki maana yake lengo lako linakua ni kutaka tangazo lako lionekane kwa watu wengi sana ili watu wengi waweze kuwa na ufahamu wa biashara yako.

Kwahiyo Kama utachagua awareness kama dhumuni la tangazo lako halafu ukawa umechagua mojawapo ya hivyo vipengele viwili tambua kwamba lengo linakua ni kuongeza ufahamu wa biashara yako na sio kupata wateja!

Tuendelee na dhumuni la pili.

CONSIDERATION

Hapa kwenye dhumuni la consideration maana yake ni kutaka kukutanishwa na watu wapya ambao bado hawana ufahamu na biashara yako.

Kwahiyo kama lengo lako ni kupata watu wapya ambao bado hawana ufahamu na biashara yako basi consideration ndio dhumuni ambalo unatakiwa uchague.

Lakini sio hivyo tu...

Utatakiwa uchague moja ya vipengele hivi...

    3. Traffic!

Ukichagua Traffic  maana yake kitendo ambacho msomaji wa tangazo lako unataka afanye baada ya kuliona au kulisoma tangazo lako ni kutoka nje ya mtandao husika (Facebook au Instagram) akufate wewe sehemu utakayokua!

Kwahiyo ukitaka watu wakufate WhatsApp au kwenye tovuti yako dhumuni lako linatakiwa liwe Traffic

Tuendelee na kipengele kingine kwenye dhumuni la consideration.

    4. Engagement!

Ukichagua engagement maana yake kitendo ambacho msomaji wa tangazo lako unataka afanye baada ya kuliona tangazo lako ni kulike page yako au kufollow Instagram account yako au kulike tangazo lako au kucomment kwenye tangazo lako au kushare tangazo lako.

Kwahiyo ukichagua dhumuni hili tangazo lako litawafikia watu ambao wana sifa na tabia ya kulike Sana, kushare Sana na kucomment Sana!

Kama lengo lako ni kuongeza followers wa page yako ya Facebook au Instagram account yako basi dhumuni la tangazo lako linatakiwa liwe hili la engagement!

Tunaelewana mpaka hapo rafiki?

    5. App Installs.

Dhumuni hili huwa linatumiwa sana na wafanyabiashara ambao wanataka watu wainstall app yao kwenye simu zao.

Kwa mfano kuna baadhi ya vitabu au novel ili uzisome hata kama ni bure lazima uinstall kwanza app yenye novel hizo kwenye simu yako.

Kwahiyo ukichagua dhumuni hili maana yake msomaji wa tangazo lako atakachokifanya baada ya kuliona tangazo lako ni anapelekwa moja kwa moja app store au play store ili aweze kuistall app hiyo ndio aanze kupata yanayopatikana kwenye app hiyo!

Kwahiyo ukichagua dhumuni hilo mtandao unachokifanya ni kulifikisha tangazo lako kwa watu ambao Wana sifa na tabia ya kuistall app kupitia matangazo kama yako.

    6. Video views.

Ukichagua dhumuni hili maana yake unachotaka msomaji wa tangazo lako afanye ni kuliangalia tangazo lako la video.

Video yako inaweza ikawa ni elimu juu ya kitu fulani.

Kwahiyo kama hitaji lako ni video yako kutazamwa na watu wengi basi dhumuni lako linatakiwa liwe hili la video views

Kwa kuchagua dhumuni hilo mtandao utaionesha video yako kwa watu wenye sifa na tabia za kuangalia video sana wakiwa mtandaoni.

    7. Lead generation

Kabla sijaelezea dhumuni hili unatakiwa uelewe maana ya lead ni Nini.

Lead ni mtu yeyote ambaye katoa taarifa zake kwako kupitia ujazaji wa fomu.

Taarifa hizo ni majina yake, namba yake ya simu na email yake n.k

Lakini ili mtu huyu ajaze fomu inatakiwa ufanye mabadilishano ya kumpatia chambo yaani elimu ya bure kwa njia ya pdf au mfumo mwingine ndio yeye aweze kujaza taarifa zake.

Kwahiyo baada ya mtu huyu kujaza na kutuma fomu inatakiwa apate chambo ambacho ni elimu ya bure.

Hivyo basi kama lengo lako ni kupata taarifa za mtu (majina yake, namba ya simu na email) bila yeye kutoka Facebook au Instagram basi dhumuni la tangazo lako inatakiwa liwe lead generation

Kwa kuchagua dhumuni hilo mtandao utakufikishia tangazo lako kwa watu wenye sifa na tabia ya kutoa taarifa zao ili baada ya hapo uanze kuwafanyia ufatiliaji (Follow up)

Tumemaliza?

Bado.

    8. Messages

Ukichagua dhumuni hili maana yake msomaji wa tangazo lako atakutumia meseji moja kwa moja messenger au WhatsApp au Instagram.

Kwahiyo chagua dhumuni hili endapo lengo lako ni mtu akutumie Meseji moja kwa moja WhatsApp au messenger au Instagram.

Sasa, kwa madhumuni 3 yaliyobaki sitaki nikuchanganye kabisa.

Haya ni madhunu ya elimu ya juu.

Kwasababu ili uweze kuchagua madhumuni haya lazima uwe na tovuti (website) yako.

Kwanini uwe na tovuti yako?

Kwasababu inatakiwa ukopi code moja inayoitwa Facebook pixel halafu uende ukaipaste kwenye tovuti yako halafu baada ya hapo code hii itatunza taarifa zote za watu wanaotoka Facebook kuja kwenye tovuti yako kwahiyo baadae wale watu ambao hawakununua au hawakufanya vile ulivyokusudia wafanye kwenye tovuti yako unawafanyia retargeting marketing.

Naona jinsi ambavyo umekunja uso maana hujanielewa.

Ndio maana sijataka kuelezea kiundani zaidi kuhusu madhuni 3 yaliyobaki.

Baada ya kuona madhumuni ya kufanya matangazo ya kulipia mtandaoni sasa tuangalie...

Namna Sahihi Ya Kuset Tangazo Lako La Kulipia Mtandaoni!

Ni rahisi sana kuset tangazo lako.

Tangazo lako unalisetia kupitia Ads manager ambayo ndio account maalum Facebook kuset matangazo ya kulipia.

Ili uweze kuset tangazo lako unafuata hatua 3 zifuatazo.

    1. Kuchagua dhumuni la tangazo lako.

    2. Kuchagua walengwa unaotaka walione tangazo lako

    3. Kubandika tangazo lenyewe litakaloonekana kwa watu wako lengwa.

Maelezo yanafuata.

1. Kuchagua dhumuni la tangazo lako.

Hatua ya kwanza kabisa ya kuset tangazo lako ni kuchagua dhumuni la tangazo lako.

Kama nilivyokwambia hapo kwenye kipengele kilichopita kwamba dhumuni la tangazo lako ni kuamua ni kitendo gani unataka mtu atakayeliona tangazo lako akifanye baada ya kuliona tangazo lako. Kwahiyo kabla ya kufanya mambo mengine kitu cha kwanza ni kuchagua dhumuni la tangazo lako.

Hakikisha unachagua dhumuni sahihi kulingana na matakwa yako.

Baada ya kuchagua dhumuni la tangazo lako inafuata hatua ya...

2. Kuchagua walengwa unaotaka walione tangazo lako

Kumbuka mtandaoni kuna mkusanyiko wa watu tofauti tofauti. Kwahiyo ili uweze kupata matokeo mazuri kwenye tangazo lako inatakiwa uchague watu ambao ungependa mtandao husika ulifikishe tangazo lako kwao na sio kwa kila mtu mpaka kwa watu ambao hawana mapendeleo yoyote kuhusu biashara yako.

Kwenye hatua hii ya pili ndio unachagua watu sahihi ambao ungependa mtandao husika ukukutanishe nao.

Mr Bokko's Ad level image

Kama unavyoona kwenye picha hiyo hapo juu. Kuna mambo kadhaa inatakiwa uyaweke sawa. Mambo hayo ni...

  • Bajeti ya tangazo lako: Hiki ni kiasi cha pesa ambacho utaulipa mtandao husika ili uweze kuliweka tangazo lako hewani.
  • Location: Hapa unachagua mikoa ambayo ungependa watu wa sehemu hiyo pekee ndio waweze kuliona tangazo lako au unaweza ukachagua Tanzania nzima.
  • Age: Hapa unachagua umri wa watu wenye sifa za kuwa wateja wako au watu sahihi kwa biashara yako.
  • Gender: Hapa unachagua jinsia ya watu sahihi unaowahitaji. Wanaweza wakawa ni waume tu au wanawake tu au wote kwa pamoja.

Tumalizie hatua ya mwisho ya kuset tangazo lako la kulipia mtandaoni.

3. Kubandika tangazo lenyewe litakaloonekana kwa watu wako lengwa.

Hii ni hatua ya mwisho ya kuset tangazo lako. Mambo ambayo utayaset hapa inategemeana na dhumuni ambalo unakuwa umelichagua kwenye hatua ya kwanza.

Tuseme kwenye hatua ya kwanza dhumuni la tangazo lako umeamua liwe Traffic, kwa dhumuni hilo yafuatayo ni mambo ambayo utatakiwa uyaweke sawa hapa kwenye hatua hii ya mwisho wa kuset tangazo lako.

Mr Bokko's Tangazo lenyewe image
  • Image (Media): Hii ni picha ambayo itatumika kwenye tangazo lako. Inatakiwa uwe na picha ambayo umeshaiandaa tayari kwa ajili ya tangazo lako.
  • Primary Text: Hili ndio tangazo lenyewe. Inatakiwa yawe maelezo ambayo yanamshawishi msomaji kufanya kile unachotaka afanye baada ya kusoma tangazo lako.
  • Headline: Hiki ni kichwa cha tangazo lako. Ni maneno kadhaa yenye kumshawishi mtu aweze kusoma tangazo zima.
  • Call To Action: Huu ni wito kwa msomaji wa tangazo lako. Inaweza ikawa ni “Learn More”, “ Call Now”, “ Contact us” n.k

Mpaka hapo unakuwa umemaliza kuset tangazo lako kitaalamu zaidi.

Tuishie hapo kwa leo? Najua umechoka lakini ngoja tumalizie kipengele kingine cha mwisho cha muhimu sana. Kipengele hicho ni...

Kwanini Ukifanya Matangazo Ya Kulipia Mtandaoni Hupati Matokeo Mazuri.

Sio mbaya nikirudia tena. Nimeshakwambia kufanya matangazo ya kulipia sio kupata wateja bali ni kukutanishwa na watu sahihi wenye sifa za kuwa wateja wako halafu ndio uwapitishe kwenye mchakato wa kuwa wateja wako.

Kwahiyo kuna mambo mengi unatakiwa uyafanye baada ya mtu kusoma tangazo lako ili kuweza kumfanya mtu huyu awe mteja wako.

Ukishindwa kufanya hivyo utakuwa unafanya matangazo yasiyokuwa na faida na kujikuta unapoteza pesa zako tu bure.

Sikiliza... Kuna mambo mengi ambayo yanapelekea usipate matokeo mazuri pindi unapofanya matangazo ya kulipia. Baadhi ya mambo hayo ni...

  • Tangazo Bovu

Nitakwambia sasa...nitakwambia badae...nitakwambia Mara Mia zaidi....

Tangazo ndio ncha ya mkuki wako katika kupata wateja mtandaoni.

Iko hivi...

Kabla mteja hajakutana na wewe au kuanza kufanya mazungumzo na wewe anaanza kwanza kusoma tangazo lako huko mtandaoni.

Kwahiyo Kama tangazo halijamshawishi mteja kufanya jambo unalolitaka wewe basi utaishia kupoteza hela bure bila matokeo yoyote .

Na kibaya zaidi ni kwamba huwezi ukaandika tangazo zuri endapo huna ujuzi wa Copywriting.

Copywriting ni ujuzi wa kuandika maandishi ya kumshawishi msomaji afanye vile utakavyo wewe.

Unachotakiwa kuelewa ni kwamba copywriting ni profession (taaluma) kabisa. Na taaluma hii haifundushwi darasani.

Kwahiyo jitahidi ujifunze ujuzi huu ili uweze kuandika matangazo mazuri na sio uishie kupoteza pesa zako kisa matangazo mabovu.

Tunaendelea na jambo jingine

  • Kukosea DHUMUNI la tangazo.

Sababu nyingine inayosababisha usipate matokeo mazuri licha ya kufanya tangazo la kulipia ni kukosea kuchagua dhumuni sahihi la tangazo lako.

Kama ulivyoweza kujifunza hapo juu kwamba dhumuni la tangazo ni kuamua kitendo ambacho unataka msomaji wa tangazo lako akifanye baada ya kuona tangazo lako. Kwa kuamua kitendo hicho unaurahisishia mtandao husika uweze kukukutanisha na watu sahihi kulingana na dhumuni la tangazo lako.

Ukikosea kuchagua dhumuni sahihi matokeo yake utakutanishwa na watu ambao sio sahihi kwa lengo la tangazo lako na mwisho wa siku hutopata matokeo mazuri.

  • Kuweka bajeti ndogo.

Sababu nyingine kwanini ukifanya matangazo ya kulipia hupati matokeo mazuri ni kuweka bajeti ndogo kwenye tangazo lako.

Tambua kwamba kufanya matangazo ya kulipia sio mchezo wa BIKO wakuweka 1000 halafu unataka ushinde milioni 100.

Huo ni uchizi.

Sasa kuna watu washageuza matangazo ya kulipia kua mchezo wakubeti.

Mtu anaweka elfu 10 halafu lengo lake ni kupata wateja 100.

Kama unafanyaga hiyvo basi sio kidogo tunahitaji tukakupime kidogo tujue Kama upo sawa au tukuombee.

Maana huo ni utani na mzaha katika biashara.

Hivi inaingia akilini kweli unataka faida ya milioni 2 tuseme halafu hela ya matangazo unaweka elfu kumi na tano (15,000/=)?

nyie watu kuweni serious basi. Na muache ndoto za mchana.

Unataka wateja wengi lazima uwe tayari kutoa hela ya kutosha kukupatia idadi ya wateja unayoitaka.

Kwa mfano unataka wateja 50 ili utengeneze faida ya 1,500,000/= halafu ukiambiwa ili upate faida hiyo tumia 200,000/= kama bajeti ya Tangazo lako unaanza kutoa macho.

Unadhani kutengeneza faida ya 1,500,000/= ni mchuzi wa dagaa?

Naomba nieleweke...

Ukitaka wateja wengi lazima uwe tayari kuweka bateji kubwa ya kukuletea hao wateja wengi unaowataka wewe.

Na ukitaka wateja wachache au kutopata wateja kabisa geuza matangazo ya kulipia kua mchezo wakubeti.

Iweke kichwa hii...

Matangazo yakulipia ni mchezo wa You get what you pay for

Nisamehe kwa kirundi changu.

Namaanisha hivi...

Matangazo ya kulipia ni mchezo wa kupata unachokilipia

Inamaanisha Nini?

Rahisi Sana.

Ukitoa pesa kubwa utapata wateja wengi wanaoendana na pesa yako na...

Ukitoa pesa ndogo utapata wateja wachache wanaoendana na pesa yako au ukose kabisa.

Tunaelewana mtu wangu?

Basi tuendelee na sababu nyingine

  • Kuuza moja kwa moja kwenye tangazo.

Hii ni moja ya sababu kubwa sana ya kwanini watu wengi wakifanya matangazo ya kulipia hawapati matokeo  mazuri.

Inatakiwa uelewe kwamba hakuna mtu anayeingia mtandaoni kwenda kununua chochote kitu.

Labda niuulize kuna siku umewahi kuingia mtandaoni kununua chochote kitu? Jibu ni hapana.

Hivyo basi kuuza moja kwa moja kwenye tangazo lako ni kosa la jinai kwasababu kunawafanya hata watu waliokuwa na lengo la kununua wakuone kama vile upo unawinda pesa zao kitu ambacho kitafanya usipate matokeo mazuri kwenye tangazo lako.

Tukimalizia sababu ya mwisho...

  • Kutojua mchakato wa kuwafanya wasomaji wa tangazo lako wawe wateja

Kama ambavyo nimekwisha kukwambia kazi ya matangazo ya kulipia ni kuulipa mtandao husika ukukutanishe wewe na watu sahihi wenye sifa za kuwa wateja wako.

Baada ya kukutanishwa na watu hao inatakiwa ujue ni nini ukifanye ili kuwafanya watu hao wawe wateja wako.

Usipojua maana yake utaishia kukutanishwa na watu wengi lakini ambao hawatakuja kuwa wateja wako kamwe.

Kwahiyo lazima ujue mchakato mzima wa kuwafanya wasomaji wa tangazo lako kuwa wateja wako.

Hitimisho:

Mpaka hapo nina uhakika una elimu ya kutosha kuhusu kufanya matangazo ya kulipia mtandaoni.

Kilichobaki ni kuyafanyia kazi uliyojifunza.

Usiishie kusoma tu. Hakikisha unayafanyia kazi ili uweze kuanza kupata matokeo uliyokuwa ukiyataka siku zote.

Njia iko mbele yako.

Kazi kwako.

Cheers,

Mr Bokko.

P.S: Kama una swali lolote au una cha kusema kuhusu post hii usisahau kukoment hapo chini.

P.P.S: Kama unapenda mafunzo zaidi kuhusu matangazo ya kulipia bofya hapa kupata maelezo zaidi.

Related Posts

Usichokijua Na Unachopaswa Kujua Kuhusu Matangazo Ya Kulipia Mtandaoni!

Usichokijua Na Unachopaswa Kujua Kuhusu Matangazo Ya Kulipia Mtandaoni!

Mr Bokko


Mr Bokko ni Social Media Marketing & Advertising Expert + Founder & CEO wa Online Marketing System Pro Co Ltd - Kampuni yenye kuwasaidia Wafanyabiashara na Wajasiriamali njia rahisi ya kutumia matangazo ya kulipia mtandaoni (Facebook & Instagram) kuweza kunasa wateja pasipo kupoteza muda na pesa kwenye njia ambazo hazifanyi kazi.

Your Signature

  • {"email":"Email address invalid","url":"Website address invalid","required":"Required field missing"}
    >
    Powered by ProofFactor - Social Proof Notifications